Ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air, imebainisha udhaifu katika uokoaji na kwamba Jeshi la Polisi Kitengo cha Wanamaji kilipewa taarifa dakika 15 baada ya tukio lakini hakikufika kwa wakati huku mlango wa ndege hiyo ukifunguliwa na wahudumu kwa kushirikiana na abiria.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ambayo imeotolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Novemba 22, 2022 imeeleza kuwa, askari hao wenye boti 400 HP inayotumika kwa shughuli za doria na uokozi, walishindwa kuitumia wakati huo kwa kuwa haikuwa bandarini na kwamba pia walishindwa kupiga mbizi kutokana na mitungi waliyokuwa nayo kukosa gesi.
Aidha ripoti hiyo imeendelea kufafanua kuwa, kuharibika sehemu ya chini ya ndege kuliruhusu maji mengi kuingia ndani kwa msukumo mkubwa na kuwafunika kwa mujibu wa ripoti hiyo na kwamba wengi wa waliofariki walikuwa siti za mbele na kati, ambao hawakuweza kufungua mikanda kwa haraka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, imefafanua kuwa uchunguzi wa mabaki, umeonyesha ilikuwaa vigumu kufungua mlango wa nyumba wa abiria wa ndege hiyo kwa kuwa tayari ulikuwa umezama ndani ya maji na hali ya hewa ya uwanja wa ndege wa Bukoba ilikuwa shwari wakati ndege inaanza safari, lakini ilibadilika ghafla kwa mvua kuanza kunyesha, mawingu mazito na upepo mkali.
Aidha, imeeleza kuwa mhudumu mmoja ndiye aliyefungua mlango wa kushoto wa abiria, akisaidiwa na abiria kuusukuma na baadhi ya manusura akiwemo mtoto mwenye miezi 18 na mama yake waliokolewa kwa njia hiyo huku Wavuvi wakifika dakika tano baadaye na waliwapakia manusura katika boti yao na abiria 24 wakiwemo wahudumu wawili walipona.
Ajali ya ndege hiyo mali ya Precision Air, ilitokea Novemba 6, 2022 ikiwa na watu 43, 39 kati yao wakiwa ni abiria, marubani wawili na wahudumu wawili ambapo 19 walifariki dunia na 24 kuokolewa baada ya kutua kwenye maji ya Ziwa Victoria umbali wa mita 500 kutoka njia ya kurukia ndege.