Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayoonesha kuwa, Watanzania wengi wanaishi katika makazi duni imefafanuliwa na Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa hakuna makazi duni (slums) nchini bali ni makazi ambayo hayajapangwa ipasavyo.
Ufafanuzi huo wa wizara umeeleza kuwa makazi duni yaliyoandikwa kwenye ripoti hiyo yana maana ya makazi ambayo hayako kwenye mpangilio.
Aidha, Ripoti ya Takwimu ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2017, imeeleza kuwa kasi ya ukuaji wa miji na uchache wa makazi kukabiliana na mahitaji hayo, imesababisha ongezeko kubwa la makaazi yasiyo kwenye mpangilio.
Maisha katika maeneo hayo, kwa mujibu wa ripoti hiyo husababisha wananchi kuwa katika hatari ya kukabiliwa na magonjwa kutokana na kutumia maji yasiyo salama.
“Kasi ya ukuaji wa miji haiendani na mchakato wa mipango miji. Hali hii imesababisha ongezeko kubwa la idadi ya watu mijini wanaoishi katika maeneo ambayo hayakupangwa ambayo yako kwenye hatari zaidi ya kimazingira,” imeeleza ripoti hiyo.
Mwaka 2015, Ripoti iliyataja majiji ya Arusha na Tanga kuongoza kwa kuwa na asilimia kubwa zaidi ya watu wanaoishi mijini ambao wako katika maeneo ambayo hayakupangwa. Arusha ilipata asilimia 80 na Tanga asilimia 79.
Maeneo mengine yaliyopata asilimia kubwa ni pamoja na Temeke (75%), Kinondoni (74%), Zanzibar (73%), Mbeya (70%), Songea (67%), Morogoro (60%) na Musoma (57%).
Aidha, kwa ubora wa nyumba, Dar es Salaam imetajwa kuongoza kwa kuwa na nyumba zilizojengwa kwa kuta za saruji na mawe, ikiwa ni 96.9%, kwa kulinganisha wastani wa 25.8% wa mikoa yote iliyosalia.
Chanzo: The Guardian