Taarifa za kiintelijensia za Marekani zimeeleza kuwa jeshi la nchi hiyo limebaini harakati za kuhamisha silaha za maangamizi za masafa mafupi za Iran kuelekea Iraq.
Imeelezwa kuwa makombora hayo yalikuwa yanaelekezwa kwenye maeneo ambayo wapo wapiganaji wa Iraq wanaofanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko nchini humo.
Hata hivyo, maafisa waandamizi wa Jeshi la Marekani wameeleza kuwa hawaamini kama Serikali ya Tehran imeamua kuanzisha vita kamili dhidi ya Marekani.
Katika hatua nyingine, taarifa kamili za Jeshi la Marekani zilizokaririwa na CNN zimeeleza kuwa Novemba, 2019 wapiganaji hao walifanya mashambulizi ya roketi kuelekea upande wa Marekani mara nyingi zaidi ya walivyowahi kufanya kabla.
Hivi karibuni, ilielezwa kuwa kuna uwezekano wa Iran kuwa tishio dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati.
“Kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa kuzingatia yaliyobainika kupitia taarifa za kiintelijensia mwezi uliopita,” CNN imemkariri afisa mmoja mwandamizi wa Marekani.
Mkuu wa Oparesheni za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati, ameeleza kuwa walifahamu Iran itajaribu kufanya jambo kwa lengo la kulipa kisasi kutokana na hatua ya Marekani na washirika wake kuiwekea vikwazo vipya kutokana na kuendeleza mpango wake wa nyuklia.