Ingawa waajiriwa hujipatia vipato tofauti kulingana na taasisi, makampuni wanayoyafanyia kazi pamoja na fani wanazojishughulisha nazo, utafiti umeonesha kazi mbili zinazolipa zaidi Tanzania kuwa ni za fani ya usimamizi wa fedha na bima.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika Tanzania bara, umeonesha kuwa wastani wa kiwango cha chini zaidi cha mshahara wa wafanyakazi katika sekta ya fedha na bima kimepanda kutoka 1.198 milioni kwa mwaka 2015 hadi Sh1.388 milioni kwa mwaka 2016.

Imeelezwa kuwa sekta hiyo hutoa mishahara mizuri zaidi kulinganisha na sekta nyingine kutokana na uhaba wa wataalam, hali inayosababisha waajiri kuongeza kiwango cha mishahara kuwavutia wafanyakazi wenye sifa stahiki.

“Kwa mfano, kuna chuo kimoja tu cha masomo ya juu Tanzania ambacho kinatoa shahada (degree) ya masuala ya Bima. Waajiri siku zote hushindana kuwapata wachache wenye sifa hiyo,” Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Britam, Stephen Lokonyo anakaririwa akitoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo.

Ripoti hiyo iliyoachiwa rasmi wiki iliyopita inaonesha kuwa wafanyakazi wanaojihusisha na sekta za utawala, ulinzi wa jamii ndio wako katika nafasi ya pili ya malipo ya juu Tanzania ambapo wana wastani wa mishahara kati ya Sh1.293 milioni kwa mwaka 2016 ukiwa umepanda kutoka wastani wa Sh997,058 kwa mwaka 2015.

Aidha, ripoti hiyo imebainisha kuwa sekta inayojihusisha na huduma za malazi na chakula ndiyo iliyoshika mkia kwa kuwa na wastani wa mishahara midogo zaidi kwa wafanyakazi.

Wafanyakazi katika sekta hiyo walipokea wastani wa Sh200,881 katika mwaka 2016 ambapo kiwango hicho kiliongezeka kwa kulinganisha na Sh.159,753 ya mwaka 2015.

Bado kuna tofauti kubwa ya mishahara kati ya wanaume na wanawake kwa ujumla ambapo wanaume wanaonekana kuwazidi wanawake, imeelezwa.

Mkhitaryan kuikosa Qarabag, ahofia usalama wake
WhatsApp, Facebook zasababisha kifo