Serikali ya Armenia imeanzisha uchunguzi maalum kufuatia taarifa za kuwepo kwa mtandao mkubwa wa biashara ya watoto wachanga nchini humo.

Sakata hilo limesababisha kukamatwa kwa mganga mkuu wa wanawake na masuala ya uzazi, mkuu wa malezi ya watoto yatima na maafisa wengine waandamizi.

Imeelezwa kuwa soko hilo haramu la kuuza watoto limekuwepo kwa kipindi cha miaka mingi sasa.

Mwanamke anayejitambulisha kama Syzan Patvakanyan mwenye umri wa miaka 35, amekuwa cheche iliyowasha moto mkubwa wa kamata-kamata ya sakata hilo, akimtafuta mwanaye akieleza kuwa madaktari walimlazimisha kumuacha hospitalini miaka 19 iliyopita.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, mwanamke huyo anakumbuka kuwa alikuwa na umri wa miaka 16 tu alipojiingiza kwenye mahusiano ya mapenzi na akapata ujauzito.   

Anasema baada ya kujifungua, madaktari walimuita na kumtaka aachane na mwanaye huyo vinginevyo watamshtaki mpenzi wake kwa kujihusisha kingono na mtoto na adhabu yake ni kali. Kwakuwa alikuwa anampenda sana mwanaume huyo aliyekuwa anamzidi miaka mitano aliamua kumlinda.

Mwanamke huyo ameeleza kuwa wawili hao walilazimishwa kusaini fomu maalum ya kueleza kuwa wamekubali kumuachia mtoto huyo.

“Nililia sana, sikutaka kabisa kusaini na kumuachia mwanangu,” AFP wanamkariri.

Ameeleza kuwa baada ya kusaini fomu hiyo na kumuacha mwanaye hospitalini alirejea nyumbani, lakini baada ya siku tatu alirudi tena hospitalini hapo na hakumkuta mwanaye.

Hata hivyo, mwanasheria wa mganga mkuu wa masuala ya wanawake na tiba ya uzazi amekana tuhuma dhidi yake. Mwanasheria wake ameeleza kuwa ni kweli alikuwa miongoni mwa waliomsaidia mwanamke huyo kujifungua kwa mujibu wa fomu zilizosainiwa lakini hawezi kumkumbuka ikiwa imepita karibu miaka 20.

Marat Kostanyan, mwanasheria anayemwakilisha Patvakanyan tangu mwaka 2013, ameeleza kuwa mtandao wa wizi wa vichanga ni mkubwa hata kuliko wa dawa za kulevya kwani unawahusisha maafisa waandamizi na wenye nguvu kwenye mfumo wa Serikali.

“Hawa Mafia wanaouza watoto wana mtandao mkubwa na wenye nguvu hata zaidi ya mtandao wa dawa za kulevya hapa nchini,” alisema Kostanyan.

Mlinzi wa hospitali moja aliyehojiwa kwa sharti la kutotajwa jina alisema kuwa wakati mwingine wazazi walikuwa wanaambiwa kuwa watoto wao ni wagonjwa sana hivyo hawapaswi kukaa nao, lakini baadaye wanapotea.

Imeelezwa kuwa kati ya mwaka 2016 na 2018 wanawake wengi wadogo waliokuwa wanataka kutoa mimba walilazimishwa kulea mimba hizo na kujifungua kisha kuachana na watoto wao ili waasiliwe.

Naibu Waziri wa uzazi, Zhanna Andreasyan ameeleza kuwa Serikali imeanza kufanya uchunguzi wa kina kuhusu masual ya kuasili watoto kwani imeonesha kuwa watoto wengi walioasiliwa walienda nje ya nchi mara nne zaidi ya walioasiliwa ndani ya nchi.

Ingawa takwimu halisi za biashara ya watoto kwa ujumla duniani haijawekwa wazi, Shirika la Kazi duniani, mwaka 2012 lilieleza kuwa takribani watoto milioni 1.2 huathirika na biashara hiyo kila mwaka.

Kwa mujibu wa mtandao wa erasechildtrafficking, katika chapisho lao la mwaka 2016 wameeleza kuwa kila mwaka watoto 300,000 huuzwa na wafanyabiashara hiyo haramu kama watumwa. Umeeleza kuwa takribani watoto 17,000 kwa mwaka hupelekwa Marekani ikiwa ni wastani wa watoto 46 kwa siku moja.

Hapa nchini Tanzania pia kumekuwa na ripoti ya watu kuiba watoto lakini Jeshi la polisi limekuwa likichukua hatua haraka na kufanikisha kupatikana kwa baadhi ya watoto.

Mfano; Machi 31, 2019, mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina la Hawa Sindai aliibiwa mtoto wake wa siku moja akitoka hospitalini. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Paul Kasabago alimtaja mtuhumiwa kwa jina la Dori Joshua mwenye umri wa miaka 20, alitumia mbinu ya kumsaidia Bi. Sindai mwanaye na baadaye alitokomea naye. Lakini Polisi walifanikiwa kumkamata na kukipata kichanga hicho kikiwa hai.

Mlinde mwanao, hakikisha unatoa taarifa kwa Mamlaka haraka unapobaini kuna namna yoyote usiyoielewa wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua. Shiriki katika kutokomeza biashara haramu ya watoto. Rejea utamaduni wetu ‘mtoto wa mwenzio na mwanao’.

Papa Francis atuma ujumbe wa pekee kwenye ibada ya Krismas
Ndege yaangukia Ghorofa na kuua 14
Wasudan washerehekea Krismasi baada ya miaka 70

Comments

comments