Jeshi la Ushirika la Marekani linaloendesha oparesheni dhidi ya kundi la kigaidi linalojiita ‘Islamic States of Iraq and Syria’ (ISIS) limefanya mashambulizi ya anga yaliyowauwa viongozi 10 waandamizi wa kundi hilo la kigaidi.

Taarifa zilizotolewa na msemaji wa majeshi ya ushirika yanayoongozwa na Marekani, Col. Steve Warren imeeleza kuwa kati ya viongozi hao 10, alikuwemo mmoja kati ya watu wa karibu zaidi wa mtu aliyetekeleza mashambulizi ya kigaidi jijini Paris Ufaransa.

Alimtaja mtu huyo kwa jina la Charaffe al Mouadan ambaye ni mmoja kati ya viongozi wa ISIS mwenye makazi yake nchini Syria ambaye amekuwa msaada mkubwa katika kupanga njama za kufanya mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Magharibi.

Warren alieleza kuwa mashambulizi hayo yalifanyika Desemba 24 mwaka huu na yamekuwa na mafanikio makubwa ya kufifisha nguvu za kundi hilo la kigaidi katika nchi za Syria na Iraq.

Majeshi hayo yamewaua maafisa wa ngazi za juu wa ISIS katika miezi ya hivi karibuni wakiwemo Mohammed Emwazi maarufu kama ‘Jihadi John’ na afisa mwandamizi anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Abu Sayyaf.

 

Ndege yagonga jengo na kuanguka katikati ya Mji wa Marekani
Profesa Maghembe amwagia Sifa Nyalandu, Aahidi kuendeleza Aliyoyaacha