Wafanyakazi walioajiriwa katika sekta mbalimbali nchini wanalipa kiasi kikubwa zaidi cha kodi ukilinganisha na waajiri wao, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka 2016/17 ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS).
Ripoti hiyo iliyochapishwa na Ofisi hiyo hivi karibuni inayoangazia Tanzania Bara inaonesha kuwa wafanyakazi tofauti na ilivyo kwa waajiri wao, hulipia kodi ya kipato cha mishahara yao (Pay as you earn – Paye) na hulipa kodi tena kupitia fedha walizopokea wanapoanza kufanya manunuzi ya huduma na bidhaa mbalimbali.
Katika mwaka husika, imeonesha kuwa wafanyakazi kwa ujumla walilipa kodi ya Sh2.27 trilioni wakati makampuni/mashirika/taasisi zilizowaajiri yalilipa kodi ya Sh1.45 trilioni..
Aidha, imebainika kuwa kiwango cha makusanyo ya ‘paye’ kwa mwaka wa fedha 2016/17 kilikuwa pungufu kwa asilimia 46.2 ya kiwango cha mwaka 2015/16.
Kadhalika, kiwango cha kodi inayotokana na matumizi/manunuzi katika mwaka husika kilifikia Sh3.09 trilioni ambapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kilikuwa Sh2.1 trilioni.
VAT ni kiwango cha fedha kinacholipwa na mlaji wakati wa anaponunua huduma/bidhaa, kiasi ambacho wafanyakazi hulipia zaidi. Baadhi ya bidhaa ambazo wafanyakazi hutumia na huwa na VAT ni pamoja na Sigara, bia (vileo), umeme na huduma za simu.