Kocha Mkuu mpya wa Simba SC ambaye anatarajiwa kutangazwa wakati wowote mwezi huu (Juni 2022), huenda akatumia muongozo wa usajili wa wachezaji wa klabu hiyo, ulioachwa na Kocha Franco Pablo Martin.
Kocha Pablo aliachana na Simba SC, baada ya kushindwa kuivusha klabu hiyo hatua ya Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, kwa kufungwa na Young Africans 1-0, Mei 28 katika Uwanja CCM Kirumba jijini Mwanza.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema Kocha Mkuu mpya atakua na nafasi hiyo, ili kufahamu madhaifu na ubora wa kikosi kwa msimu huu kuelekea msimu ujao.
Amesema wanaamini Kocha huyo akipewa muongozo ulioachwa na mwenzake, atakuwa na nafasi nzuri ya kufanikisha lengo la kukifanyia maboresho makubwa kikosi cha Simba SC, ambacho msimu ujao kinatarajiwa kuwa na muonekano tofauti.
“Kabla ya ligi kumalizika, kocha mpya atakuwa amewasili nchini tayari kwa ajili ya kutambulishwa mara baada ya kusaini mkataba.”
“Kocha huyo mara baada ya kusaini mkataba atakabidhiwa ripoti ya usajili aliyoikabidhi Pablo kwa wachezaji aliopanga kuwasajili na wale wa kuwaacha.
“Ngumu kwa kocha mpya kufanya usajili bila ya muongozo kwani hakuwa na timu, itakuwa ngumu kwake kujua upungufu wa timu, hivyo ripoti ya Pablo ndiyo itakayotumika kufanya usajili, lakini pia kocha huyo atapewa nafasi ya kufanya usajili kwa baadhi ya nafasi,” amesema Ally
Hata Hivyo Simba SC imeanza kuhusishwa na mpango wa usajili wa baadhi ya wachezaji wa ndani na nje ya Tanzania, huku wengine wakiripotiwa kumalizana na Uongozi wa Klabu hiyo, na wanasubiri kutambulishwa kwa Mashabiki na Wanachama.