Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Serikali itawasilisha bungeni Ripoti ya Tathmini ya Utendaji inayohusu ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2016/17, iliyobaini upotevu wa fedha za umma.

Waziri Mpango ameyasema hayo leo baada ya kupokea ripoti hiyo ya PPRA katika ukumbi wa Hazina Ndogo ulioko mjini Dodoma.

“Napenda niwaahidi kwamba tutafanya utaratibu unaoainishwa kisheria kuiwasilisha ripoti hii mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Lakini vilevile, ambayo ni ahadi yangu hasa kwenu ni kuyafanyia kazi mapendekezo ambayo mmeyabainisha humu ndani,” Dkt. Mpango.

Aidha, Waziri Mpango aliipongeza PPRA kwa kazi nzuri na kuitaka kukamilisha hatua ya kuzipeleka katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) taasisi 17 za umma zilizobainishwa kwenye ripoti hiyo kuwa na harufu ya rushwa kwenye manunuzi yake.

Waziri wa Fedha, Dkt. Phillip Mpango (wanne kushoto) akiwa na wajumbe wa Bodi YA wakurugenzi na wajumbe wa menejimenti ya PPRA, baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Tathmini ya Utendaji

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Dkt. Matern Lumbanga alizitaja taasisi hizo 17 kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Moshi pamoja na Wilaya za Msalala, Kibondo na Moshi.

Taasisi nyingine ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Chuo cha Ufundi Arusha, Halmashauri ya Mji wa Kahama, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Uhasibu ya Arusha (AIAA), RAS-Kilimanjaro, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Halmashauri ya Mji wa Masasi na Kituo cha Mikutano ya Kimataifa (AICC).

Katika hatua nyingine, Balozi Lumbanga alisema ukaguzi huo ulibaini kuwa kiasi cha shilingi milioni 483.44 kililipwa kwa wakandarasi kwa kazi ambazo hazikuwa zimefanyika. Taasisi zilizohusika katika hilo ni pamoja na NSSF, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

Kwa mujibu wa Balozi Lumbanga, PPRA iliingilia michakato ya zabuni tatu zenye thamani ya shilingi bilioni 42.97 baada ya kujiridhisha kuwa Serikali isingepata thamani halisi ya fedha endapo michakato hiyo ingeendelea.

Ukaguzi huo ulihusisha taasisi za umma 112.  Taasisi za umma zinazofanya manunuzi makubwa zaidi zilihusishwa ili kupata uhalisia kwa manunuzi yanayofanywa na Serikali.

Sami Khedira, Mesut Ozil watemwa timu ya taifa
Video: Mjadala wa maudhui ya kanuni za mitandao na utangazaji waanza