Matokeo ya utafiti mpya yanaonesha kuwa ukeketaji wa wasichana barani Afrika umeshuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Utafiti huo uliochapishwa kwenye Jarida la BMJ Global Health, umeonesha kushuka kwa kiwango kikubwa kwa vitendo vya ukeketaji hususan dhidi ya wasichana wenye umri chini ya miaka 14.
Vitendo hivyo vilikuwa vimeshamiri barani Afrika na sehemu nyingine duniani, vikihuishwa na tamaduni na mila potofu, huku makundi ya haki za binadamu na Serikali za nchi mbalimbali zikipinga vitendo hivyo vya kinyama na hatari kwa afya ya mwanamke.
Ukeketaji unatajwa kuwa chanzo cha maumivu makali kwa mwanamke, kuharibika kwa mfumo wa uzazi, matatizo wakati wa hedhi pamoja na matatizo mengine ya kiafya wakati wa kujifungua.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto la UNICEF, zaidi ya wanawake milioni 200 duniani kote wamefanyiwa ukeketaji. Idadi kubwa inatajwa katika bara la Afrika na Mashariki ya Kati.
Imebainika kuwa kwa kulinganisha hali ilivyokuwa miaka 1990, Afrika Mashariki imepiga hatua kubwa zaidi ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji kutoka asilimia 71% ya wasichana walio chini ya umri wa miaka 14 katika mwaka 1995 hadi 8% katika mwaka 2016.
Tanzania na kenya zimetajwa kuwa nchi ambazo zimepiga hatua zaidi Afrika Mashariki ambapo ni asilimia 3-10 ya wasichana ndio wanaokumbwa na tatizo la ukeketaji, hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kushusha takwimu za ukeketaji katika ukanda huu.