Watu watatu wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku Wizara ya Mambo ya ndani ikisema zaidi ya watu 300 wamekamatwa kufuatia maandamano ya kuipinga Serikali, nchini Kenya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga, George Rae amesema vifo hivyo vilisababishwa na mapambano kati ya Polisi na waandamanaji katika ngome ya upinzani mjini Kisumu.
“Kuna miili miwili iliyorekodiwa awali katika chumba cha kuhifadhia maiti ikiwa na majereha ya risasi, na watu 14 wamelazwa Hospitali ambapo watu hawa walipokelewa hapa pekee baada ya ghasia za maandamano kutokea,” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Muungano wa Azimio la Umoja chini ya Kiongozi wake Raila Odinga uliapa kufanya maandamano kwa siku tatu mfululizo wiki hii, na waliandaa awamu kadhaa za tukio hilo tangu mwezi Machi 2023, huku Jumuia ya Kimataifa ambayo ikiunga mkono wito wa suluhu baada ya maandamano ya awali kusababisha vifo vya zaidi ya watu 10.