Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika Mikoa 20 tayari imesajili watoto walio chini ya miaka 5 zaidi ya Milioni Sita na kufikia asilimia 55 kutoka asilimia 13 mwaka 2012 kupitia mpango mkakati wa usajili uliozinduliwa mwaka 2018 na kutoa matokeo chanya kwa sehemu nyingi nchini.
Hayo yamesemwa leo Agosti 10, 2021 na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa. Palamagamba Kabudi wakati wa maadhimisho ya nne ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika yanayoadhimishwa Agosti 10 kila mwaka huku akitaja Mkoa wa Mara na Simiyu kusajili watoto kufikia asilimia 80 kutoka asilimia 10.
Waziri Profesa Kabudi, amesema zoezi la usajili linalofanywa na RITA ni muhimu na hufanyika kote nchini ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya kuwahudumia wananchi na imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuleta matokeo makubwa ambayo pia yanategemewa kupatikana kupitia sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka ujao.
Pia amesema mpango wa Usajili wa vifo ambao unatekelezwa sambamba na usajili wa watoto utasaidia kutambua idadi ya vifo vinavyotokea nchini sababu za vifo pamoja na kuboresha huduma za Afya sehemu mbalimbali.
“licha ya kuwepo na changamoto ya janga la UVIKO-19, RITA imepiga hatua kubwa hasa katika matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma ambapo hadi sasa huduma nyingi zinazotolewa na RITA zinatolewa kwa njia ya mtandao wa simu ikiwemo huduma za usajili wa vizazi na vifo kwa kukamilisha maombi kwa njia ya kieletroniki bila kufika katika ofisi zao”. Amesema Profesa. Kabudi.
Sambamba na hayo Waziri Profesa Kabudi, amewaomba viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu waliohudhuria katika semina hiyo kuhakikisha kuwa wanatoa maoni ambayo yataboresha haki za watu wenye ulemavu na kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi wa Haki za Kisheria RITA Lina Msanga amesema maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila Agosti 10 barani Afrika yanalenga kuongeza mwamko na kasi ya wananchi ya kusajili matukio muhimu na yanafaa kupewa kipaombele kwani yanasaidia nchini kufanya mambo ya maendeleo.