Uongozi wa Klabu ya Rivers United umewasilisha Barua Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ ukiomba kubadilisha Uwanja utakaotumika kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Young Africans.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa April 23 mjini Port Harcourt, kabla ya mchezo wa Mkondo wa pili ambao utaunguruma jijini Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Nigeria zimeeleza kuwa, Uongozi wa klabu Rivers United, tayari umesilisha barua CAF, ukiomba kuutumia Uwanja wa Adekiye Amiesimaka uliopo katika Mji wa Port Harcourt huko Nigeria badala ya Uwanja wa Gods Will Akpabio ambao ulitumika kwa michezo wa Hatua ya Makundi.
Awali Uwanja wa Adekiye Amiesimaka ulifungiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kwa kushindwa kufikia vigezo vilivyowekwa na Shirikisho hilo kwa ajili ya michezo ya ngazi ya vilabu.
“Awali tulikuwa tukitumia Uwanja wa Gods Will Akpabio, lakini hivi sasa tumewaomba CAF turudi kwenye Uwanja wa Adekiye Amiesimaka uliopo katika Mji wa Port Harcourt hapa Nigeria.”
“Tunaamini kuwa maombi yetu yatakubaliwa na CAF kuutumia uwanja huo tuliouomba,” imeeleza taarifa kutoka Rivers United
Young Africans ilitinga Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikiongoza Kundi D, huku Rivers United ikimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B.