Timu ya taifa ya Scotland usiku wa kuamkia hii leo, ilishindwa kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya, baada ya kulazimisha matokeo ya sare ya mabao mawili kwa mawili dhidi ya timu ya taifa ya Poland.

Scotland walishindwa kufikia azimio hilo wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Hampden Park.

Mshambuliaji hatari wa FC Bayern Munich, Robert Lewandowski, alionekana kuwa mwiba kwa wascotish katika mchezo huo kufuatia kufunga mabao mawili kwa upande wa Poland katika dakika ya 3 na 90.

Scotland walikua wameshajiweka mguu sawa kwa kuamini huenda mambo yangemalizika vyema, kufuatia kuongoza mabao mawili kwa moja yaliyofungwa na mshambuliaji wa pembeni wa klabu ya Portsmouth, Matt Ritchie pamoja na mshambuliaji wa klabu ya Sunderland, Steven Fletcher, lakini Robert Lewandowski aliwainamisha vichwa chini mashabiki na wachezaji wa timu mwenyeji kwa kufunga bao la kusawazisha katika dakika za lala salama.

Hata hivyo, machungu ya Scotland kushindwa kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali za Ulaya za mwaka 2016, yalizidishwa na matokeo ya mchezo kati ya mabingwa wa dunia Ujerumani dhidi ya Ireland ya kaskazini ambao walichomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Kwa matokeo hayo, Scotland wapo katika nafasi ya nne, kwenye msimamo wa kundi la nne kwa kufikisha point 12, huku wakisaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Gibraltar utakaochezwa katikati ya juma lijalo.

Kundi hilo linaendelea kuongozwa na Ujerumani wenye point 19, wakifuatiwa na Poland ambao wamefungana na Ireland ya kaskazini kwa kila mmoja kufikisha point 18.

Timu ambazo zimeshafuzu kucheza fainali za kombe la Ulaya mwaka 2016 ni wenyeji Ufaransa, England, Jamuhuri ya Czech, Iceland, Austria, Ireland ya kaskazini pamoja na Ureno.

Baadhi ya matokeo ya michezo mingine ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2016.

Ireland ya kaskazini 3 – 1 Ugiriki

Ureno 1 – 0 Denmark

Georgia 4 – 0 Gibraltar

Hungary 2 – 1 Visiwa vya Faroe

Romania 1 – 1 Finland

Albania 0 – 2 Serbia

England 2 – 0 Switzerland

Lithuania 2 – 1 San Marino

Belarus 2 – 0 Luxembourg

Macedonia 0 – 1 Hispania

Video: Lowassa Alivyoiteka Arusha, Habari Kamili Iko Hapa
Liverpool Wamalizana Na Jurgen Klopp