Siku nne zikisalia kabla ya kuvaana na Al Ahly ya Misri, Kocha wa Simba SC, Roberto Oliveira Robertinho, amefichua kuwa hana hofu na wapinzani wake, huku akisisitiza amejipanga kutumia vyema udhaifu wa wamisri hao kupata ushindi katika mchezo huo.
Simba SC itavaana na Al Ahly ljumaa (Oktoba 20) katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya michuano ya African Football League (AFL), utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jjini Dar es Salaam.
Wekundu hao wa Msinnbazi wanahitaj ushindi mnono katika mechi hiyo kabla ya kwenda ugenini kurudiana na wababe hao kutoka Misri.
Akizungumzia mchezo huo, Robertinho amesema pamoja na wapinzani wake kuwa na rekodi mbalimbalí katika soka la Afrika, lakini hana hofu kwani ana kikosi bora kinachoweza kupata ushindi.
Robertinho amesema anaiandaa vyema timu yake hususan katika safu ya ulinzi na ushambuliaji kuhakikisha anawamudu vyema wapinzani wake.
“Sasa tunasuka kikosi chetu kuelekea mchezo dhidi ya Al Ahly, tunafahamu ubora wa wapinzani wetu lakini pia wana udhaifu wao hivyo hatuna hofu nao kabisa,” amesema.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema amekuwa akiinoa timu yake na kuitaka kuongeza umakini katika kujilinda pamoja na kutumia vyema nafasi watakazozipata.
“Hata sisi tumekuwa bora katika kila nafasi lakini tunapaswa kuzidisha umakini katika ulinzi kwa kutorudia makosa tuliyoyafanya katika mechi zilizopita na pia washambuliaji kutumia nafasi wanazotengeneza ili kupata ushindi,” amesema.
Naye Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba, Ahmed Ally amesema kikosi chao kina kila sababu ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.
“Tunatambua Al Ahly ni wakubwa na ni namba moja katika ubora hilo lipo wazi, tunafanya maandalizi mazuri ili kupata matokeo katika mchezo wetu ambao ni muhimu na tunaanzia nyumbani. Lazima tuutumie vyema uwanja wa nyumbani,” amesema.
Simba itaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri ilipokutana na Al Ahly katika uwanja wa nyumbani hivi karibuni.
Katika michezo miwili iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Wekundu hao wa Msimbazi walikaribisha Al Ahly. Simba SC ilishinda bao 1-0 kila mchezo.