Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera, ‘Robertinho’, amesema siri kubwa ya ushindi mnono walioupata juzi Jumamosi (Machi 18) dhidi ya Horoya AC ya Guinea kwenye mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika umetokana na maandalizi bora na Wachezaji wake kujituma kwa dakika zote 90.
Simba imejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 7-0, dhidi ya miamba hiyo kutoka nchini Guinea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil, amesema pamoja na ushindi huo lakini haikuwa kazi rahisi kutokana na ubora waliokuwa nao wapinzani wao Horoya AC ambayo inauzoefu mkubwa katika michuano hiyo.
“Natoa shukrani zangu kwa kila mmoja kuanzia uongozi wachezaji pamoja na mashabiki ambao walijitokeza kutupa sapoti siri kubwa ya ushindi wetu ni maandalizi mazuri hasa kimbinu na namna ya kucheza, kwangu mchezaji bora ni yule ambaye alikimbia bila kuwa na mpira na niliwaambia wasifanye makosa karibu na lango letu,” amesema Robertinho.
Amesema wakati wanajiandaa na mchezo huo malengo yalikuwa ni kucheza vizuri na kupata ushindi, anashukuru kuona vyote vimetimia ingawa hawawezi kubweteka kwani wanarudi kujipanga ili kufanya vizuri kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi C dhidi ya raja Casablanca ya Morocco.
“Malengo yetu yalikuwa kuingia Robo Fainali nashukuru kwa maana tumefanikiwa hilo ndio jambo zuri la kujivunia,” amesema Robertinho.
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Horoya AC, Sekou Soumah Diego ameipongeza Simba kwa ushindi walioupata na kusema walistahili kutokana na kiwango bora walichokionesha kwenye mchezo huo.