Hatimaye Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amefunguka sababu za kuushinikiza Uongozi wa klabu hiyo kusajili Mlinda Lango wa Kimataifa ambaye atakuja kusaidiana na kipa mzawa, Aishi Manula.
Robertinho ambaye kwa sasa yupo mapumzikono nchini kwao Brazil amesema, anapenda kipa ambaye atakuja kumpa changamoto Manula na kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.
Kati ya majina ambayo Kocha huyo mwenye umri wa miaka 63, amependekeza ni kipa wa Kibrazil Caique Luiz Santos da Purificacao (Ypiranga RS-Brazil), Issa Fontana (Al Hilal – Sudan), Alfred Macumu na Mudekereza (Vipers SC).
Kocha huyo, amependekeza majina hayo na kuuomba uongozi kupata saini ya mmoja kati ya walinda Lango hao ili aje kuitumikia Simba SC katika msimu wa 2023/24.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema baada ya kuachana rasmi na kipa wao Beno Kakolanya, wapo katika mchakato wa kupata nyanda mwingine kutoka nje ili kuziba pengo lake.
“Tunahitaji kufanya maboresho makubwa ndani ya kikosi chetu na kukisuka vizuri ikiwemo kufanya usajili kulingana na mapendekezo ambayo ameyatoa Kocha Robertinho,”amesema.
Ameongeza kuwa maboresho yalianza kufanyika mapema baada ya kumpa ajira Kocha Robertinho ambaye atasalia kukinoa kikosi cha timu hiyo baada ya kukaa na timu kwa muda mrefu na baadhi ya wachezaji watakaosalia ndani ya kikosi cha timu hiyo.
Manula ambaye anauguza nyama za paja, alianza kuwa nje ya uwanja kuanzia Aprili na anatarajiwa kurejea Oktoba ambapo atakosa michezo kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya ‘Super League ambayo inatarajia kufanyika mwezi Agosti, mwaka huu.