Simba SC inapiga hesabu kubwa kabla ya kukutana na Al Ahly ya Misri kwenye mchezo wa ‘African Super League’ na kuna umafia ameufanya kocha wao Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ juu ya wapinzani wao hao kisha akawapa habari nzito wachezaji wake.
Alichofanya Robertinho ni kwamba amemtuma rafiki yake mmoja ambaye ana taaluma ya ukocha akiwahi pia kufanya kazi ya maskauti wa kiufundi wa timu moja ya Saudi Arabia kwenda kuwasoma Al Ahly ikiwa inacheza nyumbani ikishinda kibabe kwa mabao 3-1 dhidi ya El Ismaily.
Ushindi huo wa Al Ahly kwa mabao hayo yaliyofungwa na mshambuliaji Percy Tau, kiungo Mohamed Taher na staa wao fundi Hussein El Shahaat umempa akili kubwa Robertinho ambaye amekiri haitakuwa rahisi lakini akatamba kwamba hata Waarabu hao wanajua kwamba hawana mchezo rahisi.
Robertinho amesema kwasasa ana taarifa za kutosha juu ya wapinzani wao hao baada ya kupata ripoti kamili kutoka kwa rafiki yake na kwamba wakati wowote atapokea pia mkanda kamili wa mchezo huo.
Robertinho ingawa amekiri kwamba Al Ahly sio timu rahisi lakini anakwenda kuandaa kikosi chake kucheza kwa akili kubwa kupata matokeo mbele ya mabingwa hao wa Barani Afrika.
Simba SC itakuwa mwenyeji wa AL Ahly Oktoba 20, katika ufunguzi wa mashindano hayo mapya ya klabu Barani Afrika, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya timu hizo kurudiana siku nne baadae.
“Nimefanya kazi nchi za Kaskazini, nina watu wengi sana kule, mimi sio kocha niliyekuja kuonekana hapa Tanzania, angalia Al Ahly mchezo wao wa mwisho waliocheza nilimtuma mtu akaenda kuangalia na ripoti yao kamili ninayo,”amesema Robertinho.
“Ukiacha kumtuma mtu nilikuwa pia naangalia hiyo mechi na sasa najua ubora wao, rafiki yangu haitakuwa mechi rahisi kwao wala kwetu nakuhakikishia tutapambana nao.
“Tutakwenda kuandaa kikosi chetu kucheza soka la malengo tupate matokeo, tuna timu bora hapa Simba, kwa sasa najua shida yao iko wapi na wako bora pia maeneo gani tunatakiwa kujipanga kuhakikisha hawachezi kwa utulivu wao.
Aidha Robertinho ameshusha mkwara akisema matokeo ya Simba SC ikiwa nyumbani sio kitu ambacho kitawapa usingizi Al Ahly watakuja wakijua kwamba wanakwenda kukutana na timu ngumu kupoteza nyumbani.
Amesema kikosi chake kitakuwa na siku 9 ngumu za kujipanga na mchezo huo ambapo tayari amewataka wachezaji wake kujiandaa kiakili kuelekea mchezo huo.
“Simba ni timu ambayo mechi zetu nne za Afrika zilizopita hatujapoteza watu hawatakiwi kusahau hili lakini pia Al Ahly walipokuja hapa mara ya mwisho wanajua kwamba hawakushinda dhidi ya hii timu, haya mambo mawili ndio yanaifanya Simba SC kuwa ndani ya klabu kumi bora Afrika na sasa tunakwenda kukutana nao mtaona sio mchezo rahisi.
“Nimewaambia wachezaji wangu hizi mechi tano tulizocheza za ligi zimetupa nguvu ya kujiandaa vizuri lakini pia mashabiki wetu wazuri watakuja kifua mbele wakijua wanakuja kuipa nguvu timu yao ambayo sio rahisi kuwaangusha, tutakuwa na siku tisa au juma moja gumu ambalo akili za wachezaji zikitulia tutaibeba heshima ya Simba na Tanzania.