Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira Robertinho’ amesema anakwenda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akijivunia ubora wa safu yake ya ushambuliaji ambayo inaundwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kufunga.
Miamba hiyo ya soka nchini itaanza kampeni ya michuano hiyo ikiwa ugenini Zambia kucheza na Power Dynamos, mchezo unaotarajia kuchezwa Uwanja wa Levy Mwanawasa Jumamosi (Septemba 16), mjini Ndola.
Akizungumza kwenye mazoezi ya timu hiyo, Kocha huyo raia wa Brazil ameeleza kuwa anaimani kubwa na washambuliaji wote aliokuwa nao kwenye kikosi chake kutokana na uwezo wao na rekodi walizonazo katika kufunga mabao.
“Huwezi kuwa bingwa au kufikia malengo kama hufungi mabao na huwezi kufunga mabao kama huna watu sahihi wa kufunga, Simba SC tuna watu sahihi wanaoijua kazi yao katika eneo hilo, tunakwenda kucheza na Power Dynamos tukiwa na uhakika wa kufunga kutokana na watu tuliokuwa nao kwenye safu ya ushambuliaji,” amesema Robertinho.
Kocha huyo amesema kwenye michuano hiyo msimu uliopita walimtegemea zaidi Jean Baleke lakini safari hii wameliboresha eneo hilo kwa kuongeza baadhi ya wachezaji akiwemo Willy Esomba Onana, Luis Miquissone na kurejea kwa Moses Phiri ambaye alikuwa mwiba kwenye mechi za hatua ya mtoano msimu uliopita.
Amesema kwa namna alivyokiandaa kikosi chake timu pinzani itakuwa na kazi kubwa ya kuwadhibiti washindwe kufunga katika mechi zao kutokana na mbinu na ubora waliokuwa nao washambuliaji wake.
Mbali na ubora wa safu yake ya ushambuliaji lakini pia kocha huyo amesema kwa ujumla kikosi chake kipo tayari kuelekea michuano hiyo ambayo lengo lao kubwa msimu huu ni kufika nusu fainali.
Kikosi cha Simba SC kinatarajia kuondoka Dar es Salaam keshokutwa Alhamis (Septemba 14) kikiwa na wachezaji 23, benchi la ufundi 10 na viongozi watakaoambatana na timu hiyo nchini Zambia.