Wakati Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akitarajiwa kupangua kikosi ili kufanya usajili wakati wa Dirisha la Usajili litakalofunguliwa baada ya msimu huu 2022/23 kufikia kikomo, Kocha huyo ameonesha kupenezwa na uwezo wa Mchezaji kiraka Erasto Edward Nyoni.
Uwezo mkubwa na namna anavyobeba majukumu ya timu kila Mchezaji huyo anapopewa nafasi, ndizo sifa ambazo zinatajwa kumvutia Kocha Robertinho, ambaye alikabidhiwa kikosi mwanzoni mwa mwaka huu akitokea Vipers SC ya Uganda.
Akizungumza juu ya mchezaji huyo mkongwe, Robertinho ametaja vitu vinne vinavyomfanya aone umuhimu wa Nyoni kuwepo kikosini, kwamba ni kuweza kuziba mapengo ya wachezaji wengine wanapokosekana, uzoefu wake unaosaidia chipukizi kujifunza, mtazamo na nidhamu aliyonayo.
Robertinho amekiri kutoumiza kichwa kumtumia Nyoni kwenye nafasi anazocheza na amekuwa aki fanya majukumu kilkamilifu, hivyo anaona ana faida kuwa na mchezaji wa namna hiyo kikosini.
“Nyoni anajitambua na anatekeleza majukumu yake kwa usahihi, inakuwa rahisi kumfikiria kumtumia wakati wowote anapohitajika, aina ya wachezaji wa aina yake ni muhimu kwenye timu.”
“Ana nidhamu ya juu, kuanzia kwenye kazi zake, mchezaji wa namna hiyo ni rahisi kukaa kwenye ramani ya kazi yake, anajua afanye nini na kwa wakati gani,” amesema kocha huyo.
Amesisitiza kuwa Nyoni ni mchezaji muhimnu kwa Simba SC kutokana na nafasi anazocheza, hivyo anaheshimu uwezo wake na anavyochukulia vitu kwa mtazamo chanya wenye manufaa kwa klabu.
“Naangalia zaidi anachokifanya uwanjani bila kujali anaanza kikosi cha kwanza ama anaingia kipindi cha pili, kikubwa ni utekelezaji wa majukumu yake kwa usahihi na maarifa makubwa.”
“Namuelezea kwasababu uzoefu wake, sina maana wengine hawawajibiki, ila lipo jambo muhimu la kujifunza kwa chipukizi ili kufanya kazi zao kwa kiwango cha juu,” amesema