Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema ana mpango wa kumtumia Kennedy Juma kwenye mechi za kimataifa kama mbadala wa Henock Inonga ambaye bado ni majeruhi.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 63 amesema sababu ya mabadiliko hayo ni kutokana na kazi nzuri anayoifanya beki huyo mzawa akishirikiana na Che Fondoh Malone.
“Kwa mechi kadhaa ambazo Kennedy amecheza baada ya Inonga kuumia ameonesha uwezo mkubwa, nadhani anaweza kuwa mbadala sahihi wa Inonga hasa katika mechi za kimataifa ambazo zinatukabili hivi karibuni,” amesema Robertinho.
Kocha huyo amesema anachokusudia kukifanya kwa wawili hao ni kuwaongezea mbinu ili wacheze kwa kuelewana na kutoruhusu mabao kama ilivyokuwa kwenye mechi mbili za ligi walizocheza hivi karibuni.
Robertinho amesema wanakwenda kukutana na timu zenye washambuliaji wenye ubora wa hali ya juu hivyo wanapaswa kuwa makini katika kila tendo wanalolifanya hasa safu ya ulinzi ndio maana anataka kuwaongezea kitu mabeki wake ili kuwa na safu imara ya ulinzi.
Mbrazili huyo amesema hana hofu na safu yake ya ushambuliaji kwani imekuwa ikitimiza wajibu wake kwa kiwango cha juu na hilo limejionesha kwenye mechi za Ligi Kuu Bara ambazo wamefunga bao katika kila mchezo.
Simba itacheza na Al Ahly ya Misri Oktoba 20, mwaka huu katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Afrika Football League (AFL) na Inonga bado hajawa fiti vya kutosha kutokana na kukaa nje muda mrefu kuuguza jeraha alilolipata kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union.