Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera Robertinho ameibuka na kutamka kuwa kiwango ambacho wamekionyesha wachezaji wake mchezo dhidi ya Tanzania Prisons kimewaziba midomo wale wote waliokuwa wakiponda hawaonyeshi kiwango bora.
Simba SC ilivaana dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi Alhamis (Oktoba 05) kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Katika mchezo huo, uliomalizika kwa Simba SC kushinda mabao 3-1, yaliyofungwa na John Bocco, Clatous Chama na Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’.
Robertinho amesema kuwa amefurahia kuona wachezaji wake wakicheza kwa kufuata maelekezo yake na sio kusikiliza kelele za mashabiki.
Robertinho amesema kuwa wachezaji wake wamecheza kwa kiwango kikubwa, walipovaana dhidi ya Prisons tofauti na ushindi walioupata, pia wametoa burudani ya soka safi na kuvutia mashabiki.
Ameongeza kwa kuwataka wachezaji wake kuendelea kucheza soka safi katika michezo ijayo, bila ya kusikia presha ya mashabiki itayowatoa mchezoni.
“Kiwango ambacho wamekionyesha wachezaji wangu juzi Alhamis kimewaziba midomo wale wote ambao wamekuwa wakiwaponda kwamba hawaonyeshi kiwango bora katika michezo iliyopita ya ligi na kimataifa.
Nafurahia kuona wachezaji wangu wakicheza kwa kufuata maelekezo yangu, na sio presha ya mashabiki na hatuchezi ilimradi tu, bali tunamtizama mpinzani wetu ana ubora gani wakati huo.
“Ninataka kuona wachezaji wangu wakiendelea kucheza kwa kiwango hicho ambacho wamekionyesha katika mchezo dhidi ya Prisons ili waendelee kuwaziba midomo mashabiki wanaowasema, amesema Robertinho.