Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema tayari ameandaa nfumo atakaotumia katika mchezo wa mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos utakaopigwa Septemba 16, Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola nchini Zambia na atawashangaza wapinzani wake hao.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema watakwenda na mfumo wao ambao anaamini utampa matokeo mazuri lakini watakuwa na nidhamu kubwa kwenye mchezo huo na watakachowapa Power Dynamos ni Suprise.
“Katika mechi yetu ya ugenini tutakwenda kucheza tofauti na tutakavyocheza nyumbani, huko tutakuwa na nidhamu kubwa ya ukabaji, kutakuwa na mstari mmoja wa mabeki, mwingine ni wa viungo wakabaji na viungo washambuliaji wote itabidi wacheze pamoja,”
“Tutacheza kwa kukaribiana na kuufinya uwanja na kama kwenye kushambulia tutakwenda kwa pamoja na kurejea haraka, baada ya hapo katika mechi ya marudiano tutaangalia nini tutafanya, lakini nyumbani tutataka kucheza kwa uhuru kila mchezaji akionyesha kipaji chake kwa sababu soka si vita ila ni sana,” amesema Robertinho.
Aidha, kocha huyo amesema anaandaa mkakati wa kuhakikisha wachezaji wake wanatumia nafasi zinazopatikana kwani amegundua wanatengeneza nafasi nyingi lakini wanashindwa kuzitumia.
“Tumecheza mechi mbili za ligi, ila mechi tulioshinda mabao 2-0 tulikosa mabao mengi tukiwa ndani ya boksi, Simba SC ni timu kubwa inatakiwa kucheza vizuri na kushinda mechi ikitumia nafasi zinazopatikana, hilo tunalifanyia kazi,” amesema Robertinho.
Aidha, Robertinho alisema kikosi chake kinatarajla kucheza mechi mbili za kirafiki na kama mambo yakienda vizuri huenda kesho Jumanosi ikateremka dimbani.
“Tunataka kulinda utimamu wa mwili na pumzi za wachezaji wetu baada ya ‘Pre Season ya nchini Uturuki, kwa maana hiyo nadhani tutakuwa na mechi kama mbili za kirafiki, Jumamosi ijayo.
Jumatatu au Jumatano, na nafikiri tutapata timu nzuri za kutupima kwa sababu tuna michuano mingi, Ligi ya Mabingwa tukiingia hatua ya makundi na African Super League tutakuwa na mechi nyingi, kwa hiyo ni lazima tujiandae vizuri,” amesema.
Katika hatua nyingine uongozi wa Simba SC upo kwenye mchakato wa kutafuta nchini jirani au sehemu sahihi ndani ya nchi kwa ajili ya kwenda kuweka kambi ya muda mfupi kabla ya kucheza mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos.