Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kinastahili heshima baada ya kuitangaza vyema nchi katika mashindano ya kimataifa.
Robertinho ametoa kauli hiyo baadaya kikosi chake kuondolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Robo Fainali kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati dhidi ya Mabingwa Watetezi Wydad AC.
Simba SC ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kumaliza dakika 90 kwa usawa wa bao 1-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mohammed V jijini Casablanca nchini Morocco.
Kocha Robertinho amesema ubora wa wachezaji wake unaonyesha Simba SC ni timu ya aina gani iliyokuwa na malengo ya kufanya vizuri katika michuano ya Kimataifa.
Amesema viwango vya juu vilivyoonyeshwa na kikosi chake katika mchezo wa marudiano dhidi ya Wydad AC vinatosha kuipa Simba SC heshima na si kubezwa.
“Timu ilikuwa katika mashindano ikichuana vikali, ilikuwa na malengo ya kuvuka Nusu Fainali kisha kucheza Fainali lakini ushindani wa soka huwa na matokeo yasiyotabirika na ndio maana safari yetu imeishia hapa,” amesema Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62
Simba SC sasa inalazimika kuhamishia nguvu zake katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambako imesaliwa na Michezo minne, huku ikiwa nyuma kwa alama tano dhidi ya vinara Young Africans wanaomiliki alama 68.
Michuano mingine ambayo Simba SC ina matarajio makubwa ya kufanya vizuri ni Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambako itacheza Nusu Fainali dhidi ya Azam FC mwishoni mwa juma hili (Jumamosi –MEI 06) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.