Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameamua kutenga programu ya mazoezi ya siku tisa sawa na saa 216, kuhakikisha anaibuka na ushindi kwenye mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC.
Simba SC itawakaribisha Mabingwa hao wa Guinea Jumamosi (Machi 18), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku mnyama akihitaji ushindi ili kujihakikishia kutinga Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mpango kazi wa kuhakikisha Horoya AC anafungwa kwenye mchezo huo ulianza baada ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Vipers SC siku ya Jumanne ya wiki hii, ambapo kikosi cha Simba SC kilipewa mapumziko ya siku moja na kurejea kambini siku ya Alhamisi.
Kikosi cha Simba SC kilianza maandalizi ya michezo yao miwili ule wa leo Jumamosi (Machi 11) dhidi ya Mtibwa Sugar na mchezo dhidi ya Horoya AC utakaopigwa Machi 18, mwaka huu.
Robertinho amesema amejipanga kutumia muda uliosalia kabla ya kukutana na Horoya AC, kwa kutumia Program maalum ambayo imeujumuisha mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Baada ya mapumziko mafupi kufuatia ushindi dhidi ya Vipers SC Jumanne, Siku ya Alhamis kikosi kilirejea rasmi kazini kuanza maandalizi mchezo ya wetu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Jumamosi (leo), lakini pia tuna programu ya siku tisa kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Horoya.”
“Kuendana na msimamo wa Kundi letu C ina maana kuwa kama tukishinda mchezo huo dhidi ya Horoya AC basi moja kwa moja tunatinga Robo Fainali, mchezo huu ni kama Fainali kwetu hivyo tunataka kuhakikisha tunafanya maandalizi makubwa.” amesema Kocha huyo kutoka nchini Brazil
Katika msimamo wa Kundi C la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Simba SC inakamatia nafasi ya pili ikiwa na alama sita, katika michezo minne waliyocheza wakishinda michezo miwili na kupoteza michezo miwili.
Raja Casablanca wanaongoza msimamo wa Kundi hiyo kwa kufikisha alama 12, ambazo zinawawezesha kufuzu moja kwa moja hatua ya Robo Fainali, huku Horoya AC ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 04 na Vipers SC inaburuza mkia kwa kuwa na alama 01.