Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ amefunguka kwa nini aliamua kumpa zawadi Mshambuliaji Kibu Dennis, baada ya mazoezi ya jana Jumatano (Januari 11).
Kibu Dennis amekua sehemu ya Wachezaji ambao walishindwa kukubalika kirahisi kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC msimu huu, kufuatia kuonesha kiwango cha kawaida kila alipopewa nafasi.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema: “Tukiwa kambini huwa tunafanya kazi kubwa na nzito, kwa hiyo inapotokea mchezaji anafanya vizuri, unapaswa kumpongeza kwa kumpa zawadi, ndivyo nilivyofanya mimi.”
“Zawadi ile nimeinunua mimi kama Kocha, na lengo langu ni kuendelea kuongoeza hamasa kwa wachezaji wangu wote ili wajitume kuanzia mazoezini hadi kwenye Michezo itakayotukabili.”
“Ninahitaji kuona tukicheza soka la ushindani na kila mchezaji awe na kiu ya kufanya vuzuri kila ninapompa nafasi, kwa hiyo nitaendelea kutoa zawadi kwa wachezaji ili waongeze bidii ya kujituma maozezini na kwenye michezo ya ushindani ili kupata matokeo mazuri.” amesema Robertinho
Simba SC imeweka kambi Dubai-Falme za Kiarabu ikijiandaa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Ikiwa huko Simba SC itacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Dhafra FC ya UAE na CSKA Moscow ya Urusi.
Simba SC itaanza kucheza mchezo wake wa kwanza wa Kirafiki kesho Ijumaa (Januari 13) dhidi ya Dhafra FC majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa za Tanzania, na Jumapili (Januari 15) itacheza dhidi ya CSKA Moscow iliyoweka kambi ya maandalizi Dubai.