Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’, amewafungia kazi Washambuliaji wake wapya akiwemo Luis Miquissone na Willy Essomba Onana kwa kuwataka wahakikishe wanaongeza nguvu ya kujituma zaidi katika kila mchezo watakaocheza kwa lengo la kupata ushindi mkubwa wa mabao.
Robertinho ametoa kauli hiyo baada ya timu hiyo kucheza michezo mitatu ya kirafiki nchini Uturuki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao.
Akizungumza mjini Ankara-Uturuki, Robertinho amesema kuwa kazi atakayoifanya katika kipindi kilichobaki cha maandalizi ya msimu mpya ni kutengeneza muunganiko wa timu kwa kuwa ana wachezaji wengi wageni ili kuweza kupata uhakika wakufunga mabao ya kutosha.
“Nataka kuona kila mchezaji wakiwemo Miquissone na Onana, Ngoma na wengine wajitume kwa asilimia zote kupata nafasi, tumesajili wachezaji wazuri kinachofuata ni kutengeneza timu yenye muunganiko imara na kuweza kupata matokeo ya ushindi katika kila mchezo ambao tutacheza.
“Walicheza vizuri kwenye kushambulia, kuzuia pamoja na kumiliki mchezo kwa muda mrefu, naona ubora wa kikosi changu, sasa ninaamini tutafanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mashindano ya ndani kwa msimu ujao,” amesema Robertinho.