Kiungo Clatous Chama na Mshambuliaji Moses Phiri, ambao ni raia wa Zambia wamekabidhiwa ‘mikoba maalumu’ ya kuhakikisha Simba SC inapata matokeo chanya katika mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Power Dynamos itakayofanyika keshokutwa Jumamosi (Septemba 16) kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa uliopo Ndola nchini humo.
Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka nchini leo Alhamis (Septemba 14) tayari kuwavaa Wazambia hao katika mechi ya kwanza ya hatua ya kwanza itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera “Robertinho”, amesema licha ya kucheza na Power Dynamos na kupata matokeo mazuri katika mechi ya kirafiki, lakini bado anahitaji kuwajua zaidi wapinzani wao ambao watakuwa nyumbani.
Robertinho amesema kazi kubwa ambayo amewapa Chama na Phiri ni kutoa siri ya Power Dynamos wanavyocheza mechi nyumbani ili waingie na mbinu itakayowasaidia kumaliza mchezo huo wa ugenini.
“Tulifanikiwa kucheza na timu hiyo kwa kushinda, ninaimani kufikia mechi ijayo watakuwa kivingine, nawatumia wachezaji wangu hawa wawili kueleza nini wanachokifahamu kwa wapinzani wetu wanapokuwa kwenye Uwanja wa nyumbani.
“Haitakuwa mechi rahisi, kama tulivyowafunga katika tamasha letu haitaleta maana wao ni wepesi, ninaimani watakuja tofauti na vile walivyocheza awali kwa sababu haya mashindano,” amesema Robertinho.
Ameongeza mchezo huo ni wa mashindano na wanataka kufanya vizuri katika mechi hizo mbili na kusonga mbele akiamini Chama na Phiri, watatoa siri za timu hiyo inapocheza nyumbani.
Kocha huyo amesema maandalizi ya timu yake yanaendelea vizuri na tayari ameyafanyia kazi mapungufu ya kila eneo na kuboresha pale walipofanya vizuri kwa kuzingatia michezo mitatu ya kirafiki waliocheza hivi karibuni.
Naye Meneja wa ldara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema maandalizi muhimu kuelekea medhi hiyo ya kimataifa yamekamilika na hakuna kitakachowazuia kutinga hatua ya makundi, kusaka robo na kufikia malengo yao ya kucheza nusu fainali.
“Tumecheza michezo mitatu ya kirafiki wakati wa maandalizi, Kocha Robertinho ameridhishwa na muunganiko wa kikosi, tupo imara, kiufundi tupo vizuri,” Ahmed amesema
Ameongeza wachezaji wote wako katika hali nzuri na nyota waliokuwa kwenye timu za taifa wamesharejea na wameungana na wenzao.
Amesema pia uongozi umefurahishwa na mwitikio mkubwa wa mashabiki waliojitokeza kwenda kuishangilia timu yao katika mechi hiyo ya kimataifa.