Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akisema kuwa kikosi chao kipo tayari kucheza na Al Ahly na kupata ushindi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Miamba hiyo ya soka imeingia kambini juma hili kujiandaa na mchezo huo wa ufunguzi dhidi ya Al Ahly ya Misri ikiwa ni ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League (AFL) inayoshirikisha timu nane pekee.
Kocha huyo amesema usajili walioufanya msimu huu pamoja na kushinda mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara, zinaonesha namna gani walivyokuwa tayari kwa mchezo huo wa ufunguzi ambapo utachezwa Oktoba 20.
“Ni kweli ni mechi ngumu sababu tunacheza na bingwa wa Afrika, lakini ugumu huo hautakuwa kwetu, bali kwa timu zote mbili na Al Ahly wanalijua hilo, Simba SC hatujapoteza mechi nne za Afrika zilizopita, mashabiki wanapaswa kulijua hilo na wasimame mstari wa mbele kujivunia timu yao,” amesema Robertinho.
Kocha huyo amesema wanazo mbinu mbadala za kuwapa matokeo mazuri hasa wanapocheza na timu kubwa kama hiyo hivyo haoni sababu ya mashabiki wao kuwa na hofu kwani uhakika wa ushindi kwenye uwanja wa nyumbani ni mkubwa tofauti na wanavyofikiria.
Amesema Simba SC ni timu kubwa na inaogopewa Afrika na wamedhamiria kuthibitisha hilo kwa kuifunga Al Ahly ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele hatua zinazofuata kwenye mashindano hayo ya AFL.
Simba SC ambao ndio vinara wa Ligi Kuu Bara hivi sasa, wanashiriki michuano hiyo ya AFL, kutokana na ubora waliouonesha kwenye mashindano ya CAF katika kipindi cha miaka minne iliyopita.