Wakati Miamba ya Soka Tanzania Simba SC na Young Africans zikitarajiwa katika kushuka dimbani wikiendi hii mashindano ya Kimataifa, makocha wa timu hizo wamepania kuhakikisha safu za ulinzi zinakuwa imara.
Young Africans na Simba SC zinatarajia kucheza michezo ya marudiano ya hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), michezo itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Simba SC itashuka dimbani keshokutwa Jumapili (Oktoba Mosi) dhidi ya Power Dynamos ya Zambia ikiwa na kumkukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza, Young Africans itacheza kesho Jumamosi (Septemba 30) dhidi ya Al Merrikh ya Sudan baada ya ushindi wa mabao 2-0 waliopata katika mchezo wa kwanza.
Kocha wa Simba Roberto Oliviera ‘Robertinho, amesema ameifua safu yake ya ulinzi vya kutosha kuhakikisha hairuhusu mabao katika mchezo huo.
Ukiacha mazoezi ya walinzi wote, kocha huyo alikuwa na program maalum na Kennedy Juma, ambaye atakabidhiwa mikoba ya Henock Inonga, ambaye ni majeruhi.
Kocha huyo amesema anahitaji kupata mabao katika mchezo huo, kabla ya walinzi alianza na washambuliaji ambao anaamini kwa asilimia kubwa wameimarika.
“Tumejiandaa kuhakikisha tunapata mabao ya kutosha na kuzuia lango letu kwa umakini, kazi yetu kubwa ni kuzuia na kuwashambulia kwa kushtukiza,” amesema.
Simba SC imeanzia hatua ya pili ya michuano hiyo na ikifanikiwa kuitoa Power Dynamons itafuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Kocha wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi, ameendelea kuinoa safu yake ya ulinzi huku akimwongeza katika kikosi Nickson Kibabage ambaye atasaidiana na Joyce Lomalisa, upande wa kushoto.
Gamondi amesema anahitaji mabao mengi zaidi kuhakikisha timu hiyo inafuzu hatua ya makundi kwa rekodi ya kipekee ikiwemo kutoruhusu kufungwa.
“Tunahitaji ushindi wa historia, tunataka kuingia makundi kwa rekodi ya pekee yetu, nawaamini nyota wangu, kikubwa mashabiki waje kushuhudia burudani.” amesema.
Young Africans ilitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 7-1 iliyoupata dhidi ya Asas FC ya Djibouti katika hatua ya kwanza.