Kocha wa Simba SC, Roberto Oliveira Robertinho amesema, anachohitaji ni kuwafunga Al Ahly leo Ijumaa (Oktoba 20) na kuweka heshima na rekodi Afrika kwa kumsimamisha kigogo wa soka la barani humo kwenye mechi ya kwanza ya African Football League.
Robertinho na Simba yake, leo Ijumaa (Oktoba 20) kwenye Uwanja wa Mkapa Dar wanakutana na mpinzani mgumu Al Ahly.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema wanamheshimu mpinzani yoyote wanayekutana naye, lakini kwa sasa kila mpinzani katika bara la Afrika anapaswa kuiheshimu Simba pia.
“Tunaheshimu kila mpinzani aliyepo mbele yetu, leo Ijumaa ni fursa nzuri kwa wachezaji wangu kucheza mechi kubwa.
“Tunaiheshimu Al Ahly kwa sababu ina wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa lakini pia kila timu inapaswa kuiheshimu Simba.
“Kama nilivyosema awali AI Ahly ni timu kubwa, ina mafanikio zaidi Afrika lakini leo tunahitaji kuonesha uwezo wetu. Kwangu mchezo wa mpira wa miguu sio kama kupigana bali ni sanaa, leo itakuwa ni mechi nzuri” amesema.
Robertinho aliwataka mashabiki wa Simba kuwa tayari kwa mchezo huo na wanapaswa kwenda kwa wingi kwenye Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya mchezo huo mkubwa Afrika na dunia kwa ujumla.