Kocha Mkuu wa Simba SC Robert Oliveira ‘Robertinho’ amefunguka kuwa wametua salama nchini Morocco wakiwa na lengo kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wudad AC.
Simba SC itaikabili Wydad AC keshokutwa Ijumaa (April 28) katika Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca, huku ikiwa na mtaji wa bao 1-0, waliloshinda katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza jijini Dar es salaam.
Kocha Robertinho amesema licha ya kutambua kuwa haitakuwa kazi nyepesi kwao kutokana na namna timu za Kiarabu zinavyocheza zikiwa kwenye viwanja vyao vya nyumbani, lakini amejipanga kupambana na kupata matokeo yatakayoivusha Simba SC hadi Nusu Fainali.
“Najua hatupaswi kuangalia matokeo ambayo tumeyapata katika mchezo wa nyumbani kwa sababu hakuna asiyejua ubora na ukubwa wa wapinzani wetu katika hii michuano na ukiangalia tunaenda kumekuja kumaliza mchezo wa mwisho hapa kwao, hawa ni mabingwa watetezi lazima tuwape heshima kwa muda wote wa mchezo.
“Lakini hatuwezi kuondoa malengo na mipango yetu ya kuhakikisha tunapata matokeo kwa sababu tunachokiangalia kuona kwa namna gani tunafikia kwenye malengo ya ushindi maana wachezaji wapo tayari kufanya kila linalowezekana matokeo mazuri yanakuwa upande wetu,” amesema Robertinho.
Katika mchezo wa Mkondo wa Pili, Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa 1-0 na kusaka ushindi mwingine, huku Wydad AC ikitakiwa kushinda kuanzia mabao 2-0 ama zaidi ili itinge Nusu Fainali.