Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameweka wazi kuwa katika wakati huu wa maandalizi ya msimu mpya (Pre Season) anataka kuhakikisha anatafuta njia mbadala ya kutoruhusu mabao kwenye safu yake ya ulinzi.
Simba SC msimu uliopita ndio ilikuwa timu iliyoruhusu mabao machache (17) katika Ligi Kuu huku ikiwa kinara kwenye ufungaji ikifunga jumla ya mabao 75.
Licha ya kuruhusu mabao hayo machache, Kocha Robertinho ameonyesha wazi bado ana kazi ya kufanya kuhakikisha msimu ujao wanaepuka kabisa kufungwa mabao mepesi.
Akizungumza baada ya kuwasili Ankara-Uturuki, Robertinho amesema kwenye kikosi chake anatafuta mzani sawa wa kuwa na wachezaji wakongwe na vijana ili kuhakikisha wanalinda mipira inayopotezwa.
“Upande wa ulinzi ni lazima siku zote uweze kuulinda mpira unaopotea, mpira wa sasa unahitaji spidi na umiliki mkubwa. Ukiweza kuumiliki mpira unakuwa na wakati mzuri wa kufanya maamuzi wapi na wakati gani uutoe.”
Robertinho amesema licha ya kuhitaji ulinzi wa kuhakikisha mipira haipotei, siri kubwa ya mpira ni kufunga kwa mabao mengi kila nafasi inapopatikana.
“Tunahitaji wachezaji wanapenda kufunga kwa sababu siri ya mpira ni kufunga, pia kwenye timu kama Simba SC inahitaji wachezaji wenye viwango vinavyofanana.
“Ukiwa na wachezaji wazuri wawili kwenye kila eneo kama itawezekana itakuwa nzuri, kumbuka msimu uliopita nikiwa na Simba SC sijapoteza mechi yoyote ya ligi na nimeshinda dabi.”
Katika hayo ni wazi mabosi wa Simba SC wanaendana na kauli ya Robertinho kwani hadi sasa tayari wameshaimalisha usajili kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji.
Eneo la ulinzi imewasajili David Kameta na Che Malone huku ikiwaongezea mikataba Mohamed Hussein Tshabalala’ na Shomari Kapombe na upande wa washambuliaji yupo Willy Onana na Aubin Kramo.