Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ yupo kwenye mipango ya kufyeka wachezaji watatu kabla dirisha la usajili halijafungwa Agosti 31.
Habari kutoka ndani ya Simba SC zinasema kuwa wachezaji ambao wameshindwa kulishawishi benchi la ufundi na sasa uongozi unafikiria kuwatoa kwa mkopo kabla dirisha halijafungwa.
Wanaotajwa kuwa katika mpango huo wa kuondoka Simba SC ni Mlinda Lango Ahmed Feruz na Mshambuliaji Mohamed Mussa, kutokana na uongozi kutaka kuwatoa kulingana na mapendekezo ya kocha ili kuliwahi dirisha la usajili lililo wazi.
“Tuna wachezaji wengi kikosini na baadhi yao hawapati nafasi kabisa, hivyo tunakusudia kuwatoa kwa mkopo ili wakaongeze uzoefu huko kwenye timu nyingine kwani bado vijana wanahitaji muda na kujifunza zaidi, lakini ndio hivyo Simba SC ni kubwa sana kwao,” kimesema chanzo hicho.
Sababu kubwa iliyoelezwa ni wachezaji hao kushindwa kuonyesha ushindani wa kutosha ndani ya kikosi na pia uongozi ukitaka wakapate muda wa kutosha kwenye vikosi vingine.
Mwanuke aliye Simba SC kwa msimu watatu, licha ya kuwa na kiwango bora lakini katika muda wote aliokaa kikosini ameshindwa kupigania namba kikosi cha kwanza na sasa anapigiwa hesabu za kutolewa kwa mkopo kati ya Namungo, KMC na Dodoma Jiji ili akapate uzoefu kisha atarejea Msimbazi.
Hali iko hivyo pia kwa kipa Feruz ambaye Simba SC inaamini katika ubora wake, lakini uwepo wa makipa wengine wanne kikosini Aishi Manula, Hussein Abel, Ayoub Lakred na Ally Salim kutamfanya akose muda mwingi wa kusafiri na timu na kucheza, hivyo viongozi wanagonga vichwa na tayari wameanzisha mazungunmzo na baadhi ya timu ikiwemo Geita Gold.
Kwa upande wa Mshambuliaji Mussa aliyejiunga na Simba SC msimu uliopita akitokea Malindi ya Zanzibar ameshindwa kulishawishi benchi la ufundi ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza, na Simba SC ina mpango wa kumpiga chini au kumrudisha kwa mkopo katika klabu yake ya zamani ya Malindi.
“Haya ni mapendekezo ya kocha, kwani anataka kuwa na wachezaji watakaoleta ushindani na hata ikitokea wenzao wana tatizo kusiwe na pengo kubwa baina yao,” kimeongeza chanzo hicho.
Akizungumza jijini Dar es salaam baada ya kuulizwa juu ya taarifa hiyo, Kocha Robertinho amesema hatatoa nafasi kwa mchezaji asiyejituma, kwani Simba SC ya msimu huu inahitaji kila Kombe hivyo hayupo tayari kumbeba mtu.
“Tuna wachezaji wengi kikosini na kama unavyoona wengi wanafanya vizuri. Siwezi kutoa nafasi kwa mtu asiyejituma na kupambana kwa ajili ya maslahi ya klabu, hii ni timu kubwa na ina malengo makubwa ambayo watu wa kuyatimiza ni wachezaji. uongozi, pamoja na sisi benchi la ufundi,” alisema kocha huyo bila kutaka kufafanua majina ya wachezaji watakaofyekwa kwa sasa.