Baada ya kutolewa kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa mikwaju ya Penati 4-3 dhidi ya Mabingwa Watetezi, Wydad AC ya Morocco, timu ya Simba SC leo inarejea kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kucheza dhidi ya Namungo FC mchezo utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Kwa zaidi ya siku 15, Simba SC haijacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu tangu ilipofanya hivyo Aprili 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ilipocheza dhidi ya watani zao wa jadi, Young Africans na kushinda mabao 2-0.
Hivyo, kwa mara ya kwanza baada ya siku hizo kupita, timu hiyo inashuka uwanjani ikiwa na kazi moja tu ya kuwaliwaza mashabiki wake kwa ushindi, huku ikijaribu kupunguza pengo la alama ilizonazo dhidi ya timu ya Young Africans inayoongoza ligi kwa alama 68.
Iwapo ikishinda, itafikisha alama 66, na itakuwa imebakisha pengo la alama mbili ambalo linaweza kubaki lilivyo au kuongezeka wakati Young Africans itakapoivaa Singida Big Stars kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kesho Alhamis (Mei 04).
Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema pamoja na kutolewa kwenye michuano ya kimataifa wachezaji wake na benchi la ufundi hawajavunjika moyo na kwamba watapambana kadri ya uwezo wao kushinda na kuwafurahisha wanachama na mashabiki wao ambao wamekuwa wakiwapa nguvu na sapoti kila wanapokwenda, wanapofanya vizuri na hata wanapoanguka.
“Tuna mechi mbili dhidi ya Namungo (leo) na Azam FC (Jumapili), tunakwenda kuzicheza zote kwa ufanisi mkubwa na kuwafurahisha wanachama na mashabiki wetu ili kusahau yaliyopita, tutacheza mechi kama zingine zote zilizopita,” alisema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi, amekiri kuwa mechi itakuwa ngumu kutokana na ubora wa Simba, lakini na wao wamejipanga kuhakikisha wanakabiliana nayo.
“Tunatambua kuwa tunacheza na timu ambayo ipo kwenye ubora wake, katika michuano ya kimataifa tumeiona, lakini kwenye ligi ipo nafasi ya pili na imekuwa inafanya vema, kwa hiyo na sisi ni lazima tuwe kwenye ubora pia.
Mpaka sasa tumejiandaa vizuri, ila changamoto tuliyonayo ni kwamba kwa siku za karibuni tumekuwa hatuko vizuri kwenye safu yetu ya ulinzi na hicho ndicho kwa kiasi kikubwa tumekifanyia kazi,” amesema kocha huyo