Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons.
Mchezo huo utachezwa baadae leo Alhamis (Oktoba 05) majira ya jioni katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, huku Tanzania Prisons akiwa mwenyeji.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema ameiandaa timu yake vizuri kwa ajili ya kupambana ndani ya dakika 90 na anaamini watavuna pointi tatu muhimu ugenini.
“Tunachohitaji ni pointi tatu bila kujali idadi ya mabao, tunaamini maandalizi tuliyoyafanya yatatusaidia kupata ushindi katika mchezo huu,” amesema.
Amesema Tanzania Prisons wanapokuwa nyumbani kwao wanakuwa imara zaidi, amechukua tahadhari zote kuhakikisha hawapotezi mchezo.
Naye Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Freddy Felix Minziro, amesema wamejjandaa vyema kupata pointi tatu katika mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka la Bongo, hasa baada ya Young Africans kupoteza jana Jumatano (Oktoba 04) dhidi ya Ihefu FC.
“Tunakwenda kucheza mpira mzuri wa ushindani, hatuangalii rekodi za nyuma tayari zilipita tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika uwanja wa nyumbani,” amesema kocha huyo.
Minziro amesema wachezaji wake wamemuahidi kupata pointi tatu katika mchezo huo.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana msimu uliopita 2022/23, Simba SC ilishinda mechi zote, ikianza kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini kabla ya kushinda mabao 7-1 katika mchezo wa mzunguko wa pili.
Wekundu wa Msimbazi wataingia katika mchezo huo, wakihitaji kuendeleza makali yao kufuatia ushindi katika michezo mitatu iliyopita, huku Prisons ikisaka ushindi wake wa kwanza msimu huu.
Katika ligi hiyo, Simba SC imeshinda mechi tatu, ikifunga Mtibwa Sugar (4-2), Dodoma Jiji (2-0) na Coastal Union (3-0), huku Tanzania Prisons ikitoka suluhu dhidi ya Singida Fountain Gate kabla ya kufungwa dhídi ya Azam (3-1) na Tabora United (3-1). Simba itaingia katika mchezo wa leo ikihitaji pointi tatu ili kuongoza ligi hiyo, kufuatia kuachwa pointi moja na kinara Azam FC ambayo juzi ilitoka suluhu dhidi ya Dodoma Jiji.
Azam FC inaongoza ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne, ikifuatiwa na Young Africans yenye pointi tisa na mechi nne, huku Simba SC ikishika nafasi ya tatu kwa pointi tisa ikicheza mechi tatu.
Kwa upande wa Tanzania Prisons, itahitaji ushindi dhidi ya Simba SC leo, ili kufikisha pointi nne ambazo zitaiwezesha kupanda hadi katika nafasi ya 12 (kabla ya mechi zingine leo).