Kuelekea mchezo dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Zambia Power Dynamos, Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera amewapa jukumu zito viungo wake.
Simba SC inatarajiwa kuvaana na timu hiyo keshokutwa Jumapili (Oktoba Mosi), katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Azam Complex, Jijini Dar es salaam.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Robertinho amesema kuwa amewataka viungo kuhakikisha wanamiliki mpira kwa muda mrefu kuanzia golini kwao kuelekea langoni kwa wapinzani.
Robertinho amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kabla ya kufika langoni kwa wapinzani wanapiga pasi nyingi kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wao.
Ameongeza kuwa anaamini viungo wake wana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira sambamba na kutengeneza nafasi nyingi za mabao hivyo kazi itakuwa rahisi kwa washambuliaji kumalizia.
Nimesikia mashabiki wakilalamika kuwa timu inapata ushindi, lakini haichezi vizuri, nimeliona hilo, nalifanyia kazi.
“Hivyo nimeanza kufanyia kazi hilo kuhakikisha wachezaji wangu wanawapa burudani mashabiki kwa soka safi la pasi.
“Nimewaambia viungo wangu wahakikishe wanafanya umiliki wa mpira muda mrefu kwa kupiga pasi na kupata ushindi ndani ya wakati mmoja.
“Ninataka kuliona kwa kuanzia mchezo ujao dhidi ya Power Dynamos ya nchini Zambia,” amesema Robertinho