Kocha Mkuu Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amefichua kuwa amerejea kwao Brazil kwa ajili ya mapumziko mafupi lakini amewaambia mabosi wa timu hiyo wasajili wachezaji ambao watakuwa na hadhi ya kucheza michuano ya Super League inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ pamoja na michuano mengine itakayokuwa mbele yao.
Robertinho ametoa kauli hiyo muda mchache kabla ya kuondoka nchini huku mabosi wa timu hiyo kupitia Bodi ya Wakurugenzi kukaa kikao cha mwisho cha kupitia mapendekezo ya Mbrazil huyo katika usajili wake wa msimu ujao.
Simba SC ni kati klabu nane ambazo zitashiriki michuano hiyo itakayoanza Agosti mwaka huu.
Taarifa kutoka SImba SC zinaeleza kuwa, Klabu hiyo imeanza kufanya usajili wa baadhi ya wachezaji waliopendekezwa na kocha huyo kabla ya kupitisha majina ya mwisho ya wachezaji anaowataka kocha huyo katika kikao cha mwisho ya usajili kilichofanyika mwishoni mwa juma lililopita.
Robertinho amesema kuwa tayari kwa upande wake ameshamalizana na uongozi wa timu hiyo juu ya wachezaji ambao anawahitaji katika kikosi chake kuelekea kwenye michuano ya Super League ili kuweza kufikia malengo ndani ya timu hiyo.
“Nadhani kwa sasa limebakia suala la uongozi kuweza kukamilisha juu ya mambo muhimu kwa wachezaji ambao nahitaji kuwa nao kwenye msimu ujao lakini najua tutaanza na michuano ya Super League sasa ni lazima wachezaji wawe wanasifa za kucheza michuano hiyo kwanza ili kufikia tunapotaka kwenda.
“Unajua hatukuwa na msimu mzuri kwa sababu hatukuweza kuchukua ubingwa wa kombe lolote sasa hayo hayakuwa malengo yetu, tunahitaji kuona tunaenda mbali zaidi msimu ujao kupitia wachezaji ambao nahitaji kuwanao kutokana na mashindano yote ambayo yapo mbele yetu,” amesema Robertinho