Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amesema mechi ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia itakuwa ya kuvutia kwa sababu timu hizo mbili tayari zinafahamiana.

Simba SC iliwaalika Power Dynamos katika Tamasha la Simba Day lililofanyika Agosti 6, mwaka huu ikiwa ni siku chache kabla ya kukutana kubaini wanaweza kukutana kwenye mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

Power Dynamos, mabingwa wa Ligi Kuu Zambia, walisonga mbele katika michuano hiyo inayofanyika kila mwaka baada ya kuwaondoa African Stars ya Namibia.

Robertinho amesema ratiba hiyo ameifurahia na hana presha yeyote kuelekea mchezo huo utakaochezwa kati ya Septemba 15 na 17, mwaka huu mjini Ndola na baadaye kurudiana hapa nchini.

Kocha huyo amesema amejiandaa kukutana na ushindani katika mechi zote mbili kwa sababu kila upande utahitaji kuonyesha ubora wake na hatimaye kutinga hatua ya makundi.

“Sina presha na mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa, nilijiandaa kukutana na timu yoyote msimu huu, hesabu zangu sio tu kutaka kuwang’oa Dynamos, bali ni kuwafunga kwao kabla ya kuja kumalizana nao katika mchezo wa marudiano,” amesema Robertinho

Ameongeza anatarajia wachezaji wake wote watashiriki katika programu za mazoezi kuelekea michuano hiyo baada ya nyota waliokuwa majeruhi, Henock Inonga na Aubin Kramo, afya zao kuimarika na wako tayari kujiunga na wenzao.

“Tuna kikosi imara sana, kitu muhimu ambacho ninafurahia ni kubakiwa na msingi wa timu yangu ya msimu uliopita, hii ni muhimu sana kwa sasa, halafu ukiongeza na hawa wapya, sina wasiwasi na timu yoyote.

“Tunawaheshimu Power Dynamos ni timu nzuri, nadhani kila mmoja anakumbuka walivyocheza na sisi hapa kwenye Simba Day, lakini Simba SC ni klabu kubwa Afrika, tunajipanga kuanza na hesabu za kushinda ugenini ili tumalizie mchezo hapa nyumbani,” amesema Robertinho.

Ajali ya moto ghorofani yauwa 73
Man Utd Kumnyakuwa Marc Cucurella