Mlinda Lango Aishi Manula huenda akaanza katika kikosi cha Simba SC kesho Jumamosi (Oktoba 14), kwenye mchezo wa Kirafiki ambao ni sehemu ya kujiandaa na mpambano wa Robo Fainali wa African Football League dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Manula amekuwa nje ya Uwanja kwa zaidi ya miezi mitano kufuatia majeraha ambayo yalimlazimisha kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini na kutoka nafasi kwa Walinda Lango wengine klabuni hapo (Ally Salim na Ayoub Lakred).
Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ amesema Manula anaendelea vizuri tangu alipoanza mazoezi na wachezaji wenzake klabuni hapo, hivyo anaamini ni muda sahihi kwake kumjaribu katika mchezo wa Kirafiki.
“Nitamjaribu Manula katika mchezo wote wa kesho, amekuwa na maendeleo mazuri tangu alipoanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake, nimefurahia kurejea kwake kwa sababu atanisaidia katika mipango yangu kuelekea katika mchezo wetu na Al Ahly” amesema Kocha huyo kutoka nchini Brazil
Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa African Football League dhidi ya Al Ahly Ijumaa (Oktoba 20), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.