Kocha Mkuu wa Simba SC, Oliveira Roberto ‘Robertinho’ amesema ameanza kuridhishwa na kiwango cha mastaa wake, huku wapinzani wao kwenye Simba Day wakiwekwa hadharani.
Simba SC juzi Jumatatu (Julai 24) ilitoka sare ya bao 1-1 na Zira FC ya Uzebaijan kwenye mchezo wa kwanza wa kirafikiri uliopigwa Uturuki ilipoweka kambi ya maandalizi ya msimu.
Robertinho aliitumia mechi hiyo, kujua kila staa ana ubora na udhaifu gani, kisha anaingia hatua nyingine ya kuongeza maarifa zaidi kwenye kikosi chake kuhakikisha kinakuwa na ushindani kila nafasi, ili msimu unaoanza uwe wa kicheko kwao.
“Nimeridhika na mechi hiyo kwani imenipa picha ya kujua uwezo wa wachezaji wangu na nini cha kuongeza zaidi, bado tunaendelea na maandalizi yatakayotuandaa kwa ushindani kwa majukumu yaliopo mbele yetu lazima wachezaji wawe fiti na viwango vya juu, hilo sina wasiwasi nalo kabisa, ndio maana nimeifurahia mechi hiyo ambayo sikulenga matokeo, bali kujua wachezaji kama wameelewa programu za mazoezi niliyowapa,” amesema kocha huyo.
Simba SC imefanya usajili wa mastaa mbalimbali wapya akiwemo Mlinda Lango Mbrazil, Jefferson Luis, Mcameroon, Che Malone Fedoh, Kiungo Mcongomani Fabrice Ngoma, mshambuliaji Onana, Muivory Coast Kramo Aubin na Luis Miquissone raia wa Msumbiji.