Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kuwa ana mbinu zote za wapinzani wao Power Dynamos, amezifanyia kazi na wapo tayari kwa mchezo wa kesho Jumamosi (Septemba 16).
Kauli hiyo ya Robertinho ameitoa wakati kikosi cha Simba SC kikiwasili salama Ndola, Zambia tayari kwa mchezo huo wa kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza baada ya kutua nchini humo, Robertinho amesena baada ya kuwasoma wapinzani wao wamegundua kuwa wana wachezaji hatari wawili, mshambuliaji mmoja na kiungo, lakini pia wanapenda kushambulia kutumia upande wa kushoto.
“Nimewasoma wapinzani wetu wana wachezaji wazuri wawili, Mshambuliaji mmoja na kiungo na wanatumia sana kushambulia upande wa kushoto, nimetengeneza vizuri kikosi changu kwa ajili ya kuwabana sehemu yao yenye nguvu hasa kiungo,”
“Simba hatuwezi kuwapa nafasi ya kuwa na mpira kwa sababu hiyo ni muhimu sana kwetu, usisahau pia wachezaji wetu wana vipaji vikubwa vya soka, hivyo nimewaambia wavitumie, watumie pia na mbinu zangu nilizowapa,” amesema kocha huyo wa zamani wa Vipers.
Kuhusu maandalizi na hali ya kikosi alisema wachezaji wake wako kwenye hali nzuri na wanasubiri mchezo tu.
“Tumejiandaa vizuri, tuna mipango mizuri kuhusu mechi hii, kila mchezaji ana furaha na yuko tayari kwa ajili ya mechi kwa sababu malengo yetu ni kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika,”
“Najua itakuwa mechi ngumu sababu tunacheza ugenini, siku zote ukicheza nje si sawa na nyumbani, pamoja na hayo nina imani na wachezaji wangu, nafikiri tutacheza vyema sana kwa sababu tuna wachezaji wenye uzoefu, tutakuwa na mashabiki wetu hapa ambao wamesafiri kuja huku kutupa sapoti,” amesema Robertinho.