Baada ya kuishuhudia timu yake ikipangwa Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amechimba mkwara mzito kuwa kama kuna mechi anaisubiri kwa hamu kubwa katika hatua hiyo ya Makundi basi ni kucheza dhidi ya Wydad Casablanca.
Mwishoni mwa juma lililopita (ljumaa-Oktoba 06) Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, liliendesha Droo ya hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa (Ligi ya Manbingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika) ambapo Simba SC walishuhudiwa wakipangwa Kundi B dhidi ya timu za Wydad Casablanca, Jwaneng Gallaxy na Asec Mimosas.
Kundi hilo linaonekana kuwa la kisasi kwa Simba SC kwa kuwa wamewahi kucheza dhidi ya timu zote huku msimu uliopita wakikutana na Wydad Casablanca katika hatua ya Robo Fainali huku kila timu ikishinda mchezo wa nyumbani kwa bao 1-0 na Simba SC kuondoshwa kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.
Robertinho amesema: “Tumefurahi kuona na kujua mapema ni timu za namna gani ambazo tunakwenda kucheza nazo katika hatua hii ya makundi, Asec Mimosas, Wydad Casablanca na Jwaneng zote ni timu bora na najua tutakuwa na michezo migumu.
“Lakini ukiniuliza mimi binafsi naweza kusema nimefurahi zaidi kwa kuwa napenda kuona tunacheza dhidi ya timu kubwa, kwa mfano nasubiri kwa hamu kubwa kucheza dhidi ya Wydad Casablanca natamani kuona tunashinda nyumbani na ugenini.”