Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kina kazi ya kudhihirisha klabu hiyo ni kubwa kwa kupata ushindi na alama tatu za kila mchezo wa Ligi Kuu.
Simba SC kesho Jumapili (Januari 22) itacheza mchezo wake wa 21 wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, ikiwa ugenini mjini Dodoma dhidi ya Dodoma Jiji FC, katika Uwanja wa Jamhuri.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jumamosi (Januari 21) Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema: “Tuna nafasi ya kuonyesha Simba SC ni timu kubwa, Baada ya kambi ya wiki moja Dubai.”
“Ili kufanikiwa tunahitaji kushinda na kuonyesha soka safi, ili kuwa mabingwa lazima kuchukua alama tatu katika kila mchezo.”
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 47, ikitanguliwa na vinara Young Africans yenye alama 53, baada ya kucheza michezo 20 ya Ligi hiyo.
Dodoma Jiji FC inayonolewa na Kocha Melis Medo kutoka nchini Marekani, ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imejikusanyia alama 21, baada ya kucheza michezo 20 msimu huu.