Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kipo tayari kuwakabili mabingwa wa Morocco, Wydad Casablanca katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika katika dimba la Benjamin Mkapa, Jumamosi (April 22).
Simba SC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mpinzani wake wa jadi Young Africans Jumapili iliyopita (April 16).
Lakini wekundu hao wa Msimbazi bado wana kumbukumbu ya kupoteza michezo miwili ya Kundi C dhidi ya wawakilishi wengine wa Morocco, Raja Casablanca.
Februari 18 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba SC walifungwa mabao 3-0 na Raja Casablanca kabla ya kufungwa tena mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika katika Jiji la Casablanca Aprili Mosi.
Robertinho amesema walishakamilisha maandalizi ya mtanange huo siku nyingi na wanachofanya sasa hivi ni kukumbushana vitu vidogo vidogo ili kuondoka na ushindi katika mchezo huo.
“Tupo tayari kwa mchezo na ninaamini tutashinda, sababu wachezaji wangu wana ari kubwa ya kupambana. Najua utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora waliokuwa nao wapinzani wetu lakini tupo tayari kwa mapambano lengo ni kupata ushindi,” amesema Robertinho
Kocha huyo Raia wa Brazil na anayesifika kwa mbinu nyingi amesema anaona wana nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali kutokana na mikakati waliyoweka kama benchi la ufundi kwa kushirikiana na uongozi wa timu hiyo.
“Tangu siku ya kwanza najiunga na Simba SC niliona kuwa tuna uwezo wa kufika mbali katika michuano hii hata fainali na hii ni kutokana na kikosi kusheheni wachezaji wenye uzoefu wa michuano mikubwa, lakini pia malengo yaliyowekwa na uongozi wa klabu hii,” amesema Robertinho anayeshikilia rekodi nzuri za kuibuka na ushindi dhidi ya Young Africans tangu akiwa na Rayon Sports ya Rwanda na baadaye Vipers ya Uganda.