Kocha Mkuu Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wala hana presha na mchezo wa marudiano akiwatumia salamu Al Ahly kuwa wanakwenda kupambana, huku akipangua kikosi.
Simba iliondoika nchini juzi Jumamosi (Oktoba 21) kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa African Football League dhidi ya Ahly ambao walilazimisha sare ya mabao 2-2 kwenye Dimba la Mkapa.
Akizungumza mjini Cairo, Misri amesema wataendelea kucheza kwa nidhamu, lakini kichwani hawazi kujilinda.
Kocha huyo amesema Simba SC itashambulia kwa akili huku ikitaka kuwa na makali ya kumalizia vizuri.
“Mimi siyo kocha wa kujilinda sijawahi kuwaza kucheza hivyo. Simba SC itacheza kwa nidhamu kubwa tukitambua ubora wa wapinzani wetu lakini tutawashambulia kwa akili,” amesema Robertinho.
“Tunaweza kuwa na mabadiliko machache ya jinsi ya upangaji wa timu lakini kitu muhimu tutaingia na akili kubwa kupigania heshima ya Simba SC.
“Kila mtu ameona mchezo wa Ijumaa (Oktoba 20), kama tulivyoanza kipindi cha pili kuna kitu tutakitengeneza. Hakuna timu isiyofungika.”
“Kuna makosa tulifanya kipindi cha kwanza. Kuna wakati tulitengeneza urahisi wa Ahly kutushambulia bila sababu za msingi. Nafahamu tulipambana na timu kubwa yenye wachezaji bora lakini tutabadilika”
Robertinho amekiri kwamba anaweza kuwa na mabadiliko ya kikosi katika mchezo huo utakaopigwa kesho Jumanne (Oktoba 24), jijini Cairo nchini.
Katika mchezo huo Simba SC inatakiwa kushinda ili iweze kutinga hatua ya Nusu Fainali.