Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kimedhamiria kupambana hadi tone la mwisho dhidi ya Mabingwa wa Uganda Vipers SC, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Hatua ya Makundi.
Simba SC itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumanne (Machi 07), ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Vipers SC iliyokuwa nyumbani Uganda.
Robertinho amesema anafahamu Vipers SC itakuja Dar es salaam kupambana zaidi ya ilivyokuwa mchezo uliopita, hivyo wanajiandaa kukabiliana na hilo, huku wakitanguliza lengo la kupata alama tatu katika Uwanja wa nyumbani.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema: “Tunakwenda kupambana na Vipers SC tukiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri, hasa baada ya kupata ushindi katika Uwanja wa ugenini juma lililopita.”
“Vipers ni timu ngumu na yenye wachezaji wazuri ambao wana uwezo wa kutoa upinzani kwa timu yoyote, hilo tunalifahamu na tutawapa heshima kubwa wakija hapa, ila halitupotezei malengo ya kupambana na kupata ushindi katika Uwanja wa nyumbani.”
“Simba SC inahitaji kushinda michezo miwili ya hapa nyumbani, kwa hiyo kila mmoja katika Benchi langu la Ufundi na Wachezaji wote tunafahamu hilo ndio kusudio kubwa kwa sasa, kwa hiyo hatutabweteka zaidi ya kupambana.”
Msimamo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika unaonesha Simba SC ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 03, ikitanguliwa na Horoya AC ya Guinea yenye alama 04, huku Raga Casablanca ikiongoza ikiwa na alama 09.
Vipers SC inayoshiriki kwa mara ya kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika inaburuza mkia wa Kundi C ikiwa na alama 01.