Uongozi wa klabu ya Liverpool umelazimika kukodi ndege maalum kwa ajili ya kuwarudisha nchini England wachezaji wao Roberto Firmino na Philippe Coutinho ambao walimaliza majukumu ya kuitumikia timu ya taifa ya Brazil mapema hii leo.
Liverpool wamelazimika kuingia gharama za kukodi ndege, ili kuwawezesha wachezaji hao kuuwahi mchezo wa mwishoni mwa juma hili, ambao utawakutanisha na mahasimu wao wa mjini Liverpool Everton FC.
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp anadaiwa kutoa msukumo mkubwa wa jambo hilo kufanyika haraka, ili kufanikisha mipango yake kuelekea mpambano wa jumamosi, ambao utakua na umuhimu kwa The Reds kupata ushindi.
Roberto Firmino na Philippe Coutinho walikua sehemu ya kikosi cha Brazil, kilichofanikiwa kuifunga Paraguay katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia, ambapo Brazil ilichomoza na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.
Hii si mara ya kwanza kwa Liverpool kukodi ndege kwa ajili ya wachezaji wao, kwani waliwahi kufanya hivyo kwa mshambuliaji Sadio Mane, saa chache baada ya timu ya taifa ya Senegal kutolewa kwenye michuano ya AFCON iliyofanyika nchini Gabon mapema mwaka huu.