Jina la aliyekua meneja wa Man City, Roberto Mancini linaongoza kwa kutajwa katika kinyang’anyiro cha kuziba nafasi ya Claudio Ranieri aliyetimuliwa na uongozi wa Leicester City usiku wa kuamkia leo.
Licha ya kuwepo kwa majina ya mameneja wengine ambao wanatajwa kuingia kwenye mchakato wa kufikiriwa kuchukua nafasi ya ukuu wa benchi la The Foxes, Mancini anaonesha kuwa na nafasi nzuri ya kufikiriwa na viongozi wa klabu hiyo ambayo imedhamiria kujiondoa kwenye harakati za kuingia kwenye shimo la kushuka daraja.
Uzoefu na ujasiri wake katika ligi ya Uingereza, vinatajwa kumbeba meneja huyo kutoka nchini Italia hasa sifa ya kuiwezesha Man City kutwaa ubingwa wa PL msimu wa 2011–12, kombe la FA 2010–11 na kombe la ligi mwaka 2012.
Wengine wanaotajwa katika kinyang’anyiro hicho Gary Rowett, Alan Pardew, Frank de Boer, Nigel Pearson na Roy Hodgson.