Kocha Roberto Martínez Montoliu amethibitisha kuachana na Timu ya Taifa ya Ubelgiji baada ya kuondolewa kwenye Fainali za Kombe la Dunia, zinazoendelea nchini Qatar.

Ubelgiji iililazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Croatia jana Alhamis (Desemba Mosi) na kufikisha alama nne, lakini ilishindwa kuzifikia alama za Croatia iliyomaliza nafasi ya pili katika msimamow a Kundi F, kwa kuwa na alama 4, ikitanguliwa na Morocco yenye alama saba, baada ya kuifunga Canada 2-1.

Martinez alitangaza maamuzi ya kuachia ngazi saa chache baada ya mchezo dhidi ya Croatia uliopigwa katika Uwanja wa Ahmad bin Ali mjini Al Rayyan, kwa kusema: “Huu ulikuwa mchezo wangu wa mwisho nikiwa na timu ya taifa ya Ubelgiji.”

“Ilikuwa safari nzuri na Ubelgiji, tulifanya kila tuliloweza ndani ya miaka sita, tulifurahisha kila mtu, kwa hivyo huu ni wakati muafaka kwangu kuondoka Ubelgiji.”

“Niliwaaga wachezaji na wafanyakazi, nilifanya uamuzi wangu kabla ya kuanza Fainali hizi za Kombe la Dunia.”

Roberto Martínez Montoliu alianza kazi ya kukinoa kikosi cha Ubelgiji mwaka 2016 akichukua nafasi ya Kocha Marc Robert Wilmots, aliyefukuzwa kazi na Shirikisho la Soka nchini humo ‘RBFA’, kufuatia kufanya vibaya kwa kikosi Ubelgiji katika Fainali za Matraifa ya Ulaya mwaka 2016.

Martínez alianza kazi kama Kocha Mkuu wa Ubelgiji Agosti 03 mwaka 2016, Mchezo wake wa Kwanza ulishuhudia Ubelgiji ikipapatuana na Hispania Septemba Mosi mwaka 2016 katika mji wa Brussels.
Katika mchezo huo Ubelgiji ilipoteza kwa kuchapwa mabao 2-0.

Hata hivyo Martinez aliweka Rekodi ya kuwa Kocha wa Kwanza wa Ulaya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 zilizofanyika nchini Urusi, kwa kuibanjua Ugiriki mabao 2-1.

Katika Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2018, Ubelgiji chini ya Kocha Martinez ilifanikiwa kushinda michezo yote ya hatua ya makundi.

Katika Hatua ya 16 bora Ubelgiji iliendelea kufanya vizuri kwa kuichapa Japan mabao 3-2, huku mchezo wa Robo Fainali ikifunga Brazil mabao 2-1 na kutinga Hatua ya Nusu Fainali, ambapo walikwama kwa kufungwa na majirani zao Ufaransa kwa kuchabangwa bao 1-0.

Ubelgiji ilimaliza Fainali za 2018 kwa kushika nafasi ya tatu, baada ya kuibanjua England mabao 2-0.

Chini ya Kocha Martínez, Ubelgiji ilipanda hadi nafasi ya kwanza katika viwango vya ubora vya FIFA kuanzia Septemba 2018 na kusalia kwenye nafasi hiyo hadi Februari 2021.

Serikali yabanwa kuwafunga wagonjwa afya ya akili
Rais Samia aipa cheti GGML mapambano ya Ukimwi